Serikali imetoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kufuata sheria na taratibu za huduma za Fedha ikiwemo kupata leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ufanisi bila kuwaumiza na kuwadhalilisha wanufaika na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka BoT Deogratias Mnyamani ametoa wito huo akizungumza wakati wa mafunzo kwa waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za Fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri.
Amesema BoT chini ya Wizara ya Fedha na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mikakati kupitia sheria ya huduma ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, ili kukomesha udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha kupitia mitandao ya simu.
“Benki Kuu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha imeona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha nchi nzima ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu namna bora ya kukopa fedha na kuweza kurejesha mkopo bila kudhalilishwa,” ameeleza Mnyamani.
Amesema mikopo inayotolewa kwa njia ya mitandao ya simu imekuwa changamoto kubwa hasa katika ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji jambo linalopelekea watoa huduma hao kuvunja sheria ya usiri inayotakiwa katika kupata huduma ya fedha kwa kuwadhalilisha wakopaji hao kwa kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu na jamaa waliochukua mikopo hiyo.
“Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania tunahitaji kushirikisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu na Polisi ili kuona namna ambayo tunaweza kulitatua suala hili la udhalilishaji linalofanywa na watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu,’’ amesema Mnyamani.
Ameongeza kuwa Wizara ya Fedha kupitia BoT hivi karibuni itaendesha kampeni kupitia vyombo vya habari na njia mbali mbali za kutoa elimu kwa umma ili kujenga uelewa kwa wananchi na watoa huduma ndogo za fedha kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika utoaji na upatikanaji wa huduma ndogo za fedha nchini.