Home BENKI Riba ya Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kuwa asilimia 6

Riba ya Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kuwa asilimia 6

0 comment 34 views

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema haya Januari 08, 2025 jijini Dar es Salaam mbele ya wakuu wa benki na taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari kufuatia kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha kilichofanyika Januari 08, 2025.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba.

“Uamuzi huo wa Kamati wa kutokubadili Riba ya BoT unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia 5, na kuwezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia takriban asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025,” amesema Gavana Tutuba.

Aidha, uamuzi huo ambao umefikiwa kutokana na tathmini iliyofanywa ya mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini, unalenga kuwa na utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni ili kuendelea kuwa na mfumuko wa bei mdogo.

“Utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni utachangia katika juhudi za kufanya wananchi kutofanya miamala kwa kutumia fedha za kigeni nchini,” ameeleza Gavana Tutuba.

Kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imesema ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) zinaonesha ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuwa imara katika mwaka 2024.

Aidha, mazingira ya uchumi duniani katika robo ya nne ya mwaka 2024 yaliimarika kwa kiwango kikubwa, ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi iliongezeka, mfumuko wa bei uliendelea kupungua katika nchi nyingi, na mazingira ya upatikanaji wa fedha kwa riba nafuu katika masoko yaliimarika.

Hata hivyo, matarajio hayo mazuri ya uchumi yanaweza kuathirika endapo migogoro ya kisiasa duniani na mivutano ya kibiashara itaongezeka.

Akielezea hali ya mwenendo wa uchumi pamoja na matarajio yake amesema uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar umendelea kuwa imara kwa mwaka 2024.

“uchumi wa Tanzania Bara ulikuwa kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza yam waka 2024, na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya nne yam waka 2024.

Kwa kuzingatia mwenendo huo, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwa sawia na maoteo ya ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2024,” amesema Gavana.

Ameeleza kuwa ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la shughuli za kilimo, usafirishaji, ujenzi na biashara.

Kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikuwa kwa ailimia 6.8 katika robo ya kwanza na asilimia 7.2 katika robo ya pili yam waka 2024 na unakadiriwa kukua kwa viwango hivyo kwa robo mbili zinazofuata, hivyokufikia maoteo ya ukuaji wa asilimia 7.2 kwa mwaka 2024.

Amezitaja shughuli zilizochangia Zaidi ukuaji huo kuwa ni utalii, ujenzi na viwanda.

Ameeleza kuwa, katika mwaka 2025, ukuaji wa uchumi Tanzania Bara na Zanzibar unatarajiwa kuendele kuwa wa kasi ya kuridhisha kwa takribani asilimia 6 na asilimia 6.8 mtawalia.

“Ukuaji huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko lwa uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati ya uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti,” ameeleza Gavana Tutuba.

Akizungumzia mfumuko wa bei amesema uliendelea kuwa tulivu katika kipindi chote cha mwaka 2024 ukiwa chini ya lengo la asilimia 5 kwa Tanzania Bara na kukaribia lengo hilo kwa upande wa Zanzibar.

“Katika robo ya nne yam waka 2024, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3 kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha, utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na kupungua j=ka bei za bidhaa katika soko la dunia hususani mafuta ghafi.

Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.5 mwezi Novemba 2024,” ameeleza Gavana wa BoT.

Amebainisha kuwa, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.1 na asilimia 4.

Ameeleza kuwa hali hiyo itatokana na kuendelea kuwepo kwa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia hususani mafuta ghafi.

“Uwezekano wa mabadiliko katika maoteo haya ni mdogo,” amesema Gavana.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter