Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tanzania, Rwanda kuimarisha biashara

Tanzania, Rwanda kuimarisha biashara

0 comment 42 views

Mawaziri wa Tanzania na Rwanda wamekutana na kujadili mbinu bora zaidi ya usafirishaji mafuta ili bidhaa hiyo iweze kufika Rwanda kwa wakati. Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es salaam, mawaziri waliokutana ni Waziri wa Miundombinu wa Rwanda Balozi Claver Gatete, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe pamoja na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani.

Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Waziri Kamwelwe ameeleza kuwa, wamekutana na kiongozi huyo kutoka Rwanda ili kuona namna bora zaidi ya kusafirisha mafuta kwa kutumia reli na Bandari za Dar es salaam, Mwanza na Bukoba huku akiongeza kuwa, wamefanikiwa kuunda timu kwa ushirikiano wa nchi zote mbili kufanya utafiti wa kina na kuangalia njia bora zaidi ya usafirishaji.

“Wamekuwa wakibeba mizigo yao kwa kutumia malori kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi Rwanda, lakini kwa kuwa tunayo miundombinu mizuri ya reli basi tunataka ianze kutumika kusafirisha mizigo hiyo. Tutaweka miundombinu ya matenki pamoja na bandari kavu katika Bandari ya Bukoba ili shehena ya mizigo inayokwenda nchi ya Rwanda zichukuliwe katika bandari hiyo”. Ameeleza Waziri Kamwelwe.

Kwa upande wake, Balozi Gatete wa Rwanda amesema lengo kuu ni kuimarisha uhusiano mzuri wa biashara uliopo baina ya mataifa hayo mawili.

“Hapa tumejadiliana jinsi ya kutumia bandari ya Bukoba kusafirisha mizigo yetu, njia hii ni fupi zaidi ikilinganishwa na ya kutoka Bandari za Dar es salaam au Mombasa hadi Kigali, Rwanda na hivyo kuwa na faida kubwa zaidi kiuchumi”. Amesema Balozi Gatete.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter