Wabunge kutoka Bunge la Zambia wametembelea Stesheni ya Magufuli Jijini Dar es Salaam kwaajili ya kujionea maendeleo ya mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) unaoendeshwa kwa umeme, ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya mafunzo na kubadilishana uzoefu katika sekta ya usafirishaji na miundombinu.
Ujumbe huo umetembelea mradi huo Mei 26, 2015, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala wa Mitaa, Makazi na Masuala ya Machifu Twaambo Mutinta.
Wabunge hao, wamepokelewa na viongozi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambao waliwapa maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa mradi huo mkubwa, mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, changamoto zinazokabili mradi huo, pamoja na matarajio ya baadaye ya usafiri wa reli nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo, wabunge wa Bunge la Zambia walipata fursa ya kutembelea miundombinu ya kisasa ya stesheni hiyo, kuangalia treni za umeme zinazotarajiwa kutoa huduma za abiria na baadae mizigo kwa kasi na ufanisi mkubwa, pamoja na kushuhudia teknolojia mpya inayotumika katika uendeshaji wa reli hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo, Mutinta amesema wamevutiwa sana na hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika kuimarisha usafiri wa reli, na kuongeza kuwa mafanikio hayo ni mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ya Afrika yanayotaka kukuza uchumi kupitia miundombinu bora ya usafiri.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Senzige Kasenge ameelezea kuwa ujio wa wabunge hao ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili, na akaahidi kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Zambia na nchi nyingine katika kubadilishana uzoefu na teknolojia ili kuendeleza sekta ya reli katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mradi wa reli ya SGR, ambao unajengwa kwa viwango vya kimataifa, unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi nchi jirani za Zambia, Congo na Burundi.