Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza viongozi wa Mkoa wa Simiyu wasiwabane wajasiriamali, wawaelimishe na kuwapa miongozo ili wajiendeleze kiuchumi.
Majaliwa alitoa agizo hilo Machi 26, 2023 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Mji wa Bariadi katika eneo la stendi ya zamani akiwa njiani kwenda Maswa.
Alitoa kauli hiyo akilenga biashara ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari madogo aina ya probox ambayo yalikuwa yamezuiliwa na uongozi wa mkoa huo.
“Viongozi nimewaomba msiwabane vijana wajasiriamali, msiwazuie kujiendeleza kiuchumi, cha msingi wapeni miongozo, wapeni elimu. Na vijana ni lazima mzigatie usalama wa gari na abiria na kufuata sheria zilizowekwa,” amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa “Mkuu wa Mkoa, ofisi yako ilisitisha matumizi ya magari haya maarufu kwa jina la mchomoko na sasa tumefungua milango. Mheshimiwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan alikwishaelekeza kuwa hawa wajasiamali wadogo wawezeshwe.” Pia ameagiza stendi kuu ya mabasi katika mji wa Bariadi mkoani humo ianze kutumika kwa mabasi makubwa na madogo ili kuondoa usumbufu kwa abiria.
“Mkuu wa Mkoa wekeni utaratibu utakaofaa ili mabasi yaanzie pale na kuishia pale lakini haimaanishi kuwa muwapitilize abiria wanaoshukia au kupandia njiani,” alisema Majaliwa.
Jana nilitembelea pale stendi kuu na kuona fedha za Serikali zinapotea bure. Kuna vibanda 148 vya wajasiriamali lakini hawafanyi kazi kwa sababu hakuna abiria wanaoingia na kutoka.
Kuna vijana wa bajaji na bodaboda wamejipanga vizuri lakini hawana kazi kwa sababu hakuna mabasi,” amesema Waziri Mkuu.