Home FEDHA Viashiria vya kukua uchumi vyatajwa

Viashiria vya kukua uchumi vyatajwa

0 comment 128 views

Yawezekana ukawa ni miongoni mwa watu wanaosikia takwimu zikielezwa kuwa uchumi wa nchi umeshuka au kupanda lakini haujui ni vigezo gani vinavyotumika katika kupima au kuonyesha uchumi wa nchi umekuwa au kushuka.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji ameweza kuvitaja viashiria mbalimbali vinavyotumika kuonyesha ukuaji uchumi wa taifa lolote duniani.

Akitoa ufafanuzi wa swali lililoulizwa na Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji Bungeni Bungeni Dodoma Naibu Waziri ametaja viashiria hivyo kwa mujibu wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa kuwa ni kuongezeka kwa pato la taifa, kuongezeka kwa pato la wastani la mwananchi kwa mwaka, kuongezeka kwa uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa ya huduma kutoka nje ya nchi.

Viashiria vingine alivyovitaja ni utulivu wa bei za bidhaa na huduma katika nchi, uwepo wa utulivu wa viwango vya kubadili fedha za kigeni, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kuongezeka kwa makusanyo ya serikali kwa ajili ya kugharamia shughuli za kimaendeleo na huduma za kijamii.

Vilevile alieleza kuwa, uwekezaji unaofanyika katika nchi ni kigezo cha msingi cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa huongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na huduma, ajira, kipato cha mwananchi mmoja mmoja na pato la Taifa hivyo kupunguza umaskini katika jamii.

Dk. Kijaji amebainisha kuwa, mchango wa Serikali katika ukuaji wa uchumi ni pamoja na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuwekeza zaidi kwenye shughuli zinazochochea ukuaji wa uchumi, kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji wa bidhaa na huduma nchini.

Dk. Kijaji amesema kuwepo kwa fedha za mzunguko katika shughuli za uchumi ni moja ya viashiria vinavyoonyesha kuporomoka kwa uchumi na kuishukuru Benki ku ya Tanzania kwa namna ambavyo imekuwa ikisimamia vyema masuala ya fedha ili kuimarisha uchumi na kuongeza kuwa, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi tatu mwananchama wa SADC zilizotajwa katika mkutano ulioanza Agosti 14 ya mwaka huu.

“Uchumi wa Tanzania unakua kutokana na hali halisi na takwimu zilizopo, ambapo katika Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) uliofanyika hivi karibuni ulieleza kuwa nchi nyingi mwanachama wa Jumuiya hiyo hazijafanikiwa katika ukuaji wa viashiria vya uchumi mkubwa isipokuwa nchi ya Botswana, Lesotho na Tanzania”.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter